SIKU ya Wapendanao (Valentien’s Day), imekuwa ikiadhimishwa kila ifikapo Februari 14 ya kila mwaka ambapo wapendao wamekuwa wakiitumia kuwaonyesha wenza au jamaa zao ni vipi wanawapenda.
Valentien’s Day imekuwa ikipata umaarufu mwaka hadi mwaka kuanzia mataifa ya Ulaya, Amerika, Asia hadi Afrika ikiwamo Tanzania.
Kwa hapa nchini, wapendanao wamekuwa wakitumiana zawadi kuonyesha jinsi wanavyopendana, wakitoana ‘out’ kwa ajili ya chakula cha mchana au usiku au hata kupata vinywaji.
Lakini pia, kumekuwa na utamaduni wa kupeana zawadi za maua mekundu ili kuonyeshana upendo, kiasi kwamba inapotokea mmojawapo hajafanya hivyo kwa mwenza wake, huwa tatizo.
Ni kwa kipindi hiki ndipo unapopita katika maduka mbalimbali ya zawadi, utakutana na idadi kubwa ya watu wakinunua maua mekundu na kadi za Valentine’s Day zilizoandikwa ujumbe mtamu wa kimahaba.
Ni kutokana na utamaduni huo, wafanyabiashara wa maua na kadi, wamekuwa wakiisubiri kwa hamu kubwa siku hiyo kama ilivyo kwa Sikukuu za Krismasi, Pasaka, Eid El Fitri na Eid El Haji.
Lakini kwa upande mwingine, kutokana na utamaduni unaoambatana na siku hiyo, mara kadhaa Valentine’s Day imekuwa ikiacha kilio kwa wapendanao.
Unajua ni kwanini? Imekuwa ikifahamika kuwa siku hiyo ndiyo hasa ambayo mtu anatakiwa kuonyesha upendo wa dhati kwa mwenza wake kwa kumpa zawadi na kuwa naye karibu kwa muda wote.
Hivyo, inapotokea siku hiyo hukuonana na mpenzi wako, hata kama amekupa zawadi zenye gharama kiasi gani, bado hutakuwa na imani naye kwa kuamini lazima alikuwa na mwingine anayempenda zaidi yako.
Hilo linatokana na imani kuwa siku hiyo kila mmoja lazima awe na yule anayempenda zaidi, hivyo kama mpenzi wako hatakuwa nawe, lazima atakuwa na mwingine.
Ni kutokana na hali hiyo, wengi wamejikuta wakiwapoteza wawapendao kutokana na ugomvi uliosababishwa na Valentine’s Day baada ya kuwakosa wapenzi wao siku hiyo.
Hata hivyo, japo wengi wanaamini siku hiyo ni mahsusi kwa wale wenye uhusiano wa kimapenzi, lakini ukweli ni kwamba tunaweza kuiadhimisha Valentine’s Day kwa kuwaonyesha upendo wale tunaowajali, yaani familia, jamaa na hata majirani zetu.
Hilo unaweza kulitekeleza kwa kuwatembelea wagonjwa huko mahospitalini, kuwatembelea yatima na wengineo wenye kuhitaji.
Nini chimbuko la Valentine’s Day?
Asili ya siku ya wapendanao ‘Valentine’s Day’ ni St Valentine, Mhubiri wa Kikristo aliyekuwa akiishi karibu na Mji wa Roma katika karne ya tatu wakati wa utawala wa Claudis II.
Claudis alitaka awe na jeshi kubwa akategemea vijana wangejitolea na kujiunga na jeshi lake.
Lakini vijana wengi hawakupenda vita kwa kuwa hawakutaka kuziacha familia zao na watoto wao.
Claudis akafikiria akaona hawa vijana kuwakomesha waingie jeshini, ni kupiga marufuku watu kuoana. Kuanzia hapo akapiga marufuku watu kuoana akitegemea vijana hawatajali sasa kujiunga na jeshi kwa sababu ya familia zao.
Askofu Valentine naye akawa anawafungisha ndoa kwa siri vijana hao.
Claudius aliposikia habari hizo, aliamuru Valentine akamatwe na akahukumiwa adhabu ya kifo cha kunyongwa.
Wakati akiwa jela akisubiri siku yake ya kunyongwa, Valentine alikuwa akitembelewa na vijana waliokuwa wakimpelekea maua kuonyesha wako pamoja naye.
Mmoja wa vijana waliokuwa wakienda kumtembelea ni mtoto wa mkuu wa gereza ambaye aliruhusiwa kuingia mpaka kwenye selo la Valentine ‘kupiga naye stori’.
Inasemekana kwamba Valentine aliangukia katika mapenzi na binti huyo wa mkuu wa gereza wakati anasubiria kunyongwa.
Inasemekana kwamba muda mchache kabla hajanyongwa, Valentine aliomba kalamu na karatasi na kuandika meseji yake ya kuaga akiweka sahihi ‘From Your Valentine’ (kutoka kwa Valentine wako).
Valentine akanyongwa Februari 14, mwaka 269 AD. Baada ya kunyongwa kwa Valentine, vijana wa Roma walianza kumuiga Valentine na kuwaandikia na kuwatumia wanawake waliowapenda salamu za mapenzi.
Tangu siku hiyo tarehe hiyo ikaanza kuhusishwa urafiki, upendo na mahaba duniani, huku ikihusishwa zaidi na mambo ya mapenzi.
Nawatakia kila la heri katika siku hii ya wapendanao.

No comments:
Post a Comment